Bellamy kuichezea Cardiff

Craig Bellamy
Image caption Kapteni wa Wales huenda akaichezea Cardiff

Klabu ya Manchester City imemruhusu mshambulizi Craig Bellamy kufanya mazoezi na Cardiff City, na kusambaza uvumi kwamba huenda akaazimwa na klabu hiyo inayoshiriki katika mechi za Championship.

Cardiff imesema "itapenda sana" kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, na ambaye inaelekea umaarufu wake umepungua katika Man City, klabu ambayo imetumia pesa nyingi katika usajili.

Bellamy anatazamiwa kujiunga na Cardiff City, kwa kipindi cha miezi sita, baada ya meneja Roberto Mancini kukosa kumsajili katika kikosi chake cha wachezaji 25 watakaoshiriki katika mechi za ligi ya Premier.

Fulham na mabingwa wa Uskochi, Celtic, pia wana nia ya kumsajili Bellamy.

Msemaji wa Cardiff ameelezea kwamba kutokana na vilabu vikubwa ambavyo vinakusudia kumsajili, ni fahari kwao kwamba huenda mchezaji huyo akajiunga na timu yao.

Bellamy wiki iliyopita alitangaza kwamba atafikiria kustaafu kabisa kutoka soka, ikiwa Roberto Mancini hatamchukua kukichezea kikosi chake.

Meneja huyo wa Man City baada ya kutomchagua katika kikosi cha watakaocheza mechi za ligi ya Premier, na wengine 23 watakoshiriki katika ligi ya Europa, alisema itafaa ikiwa Bellamy atatafuta klabu kingine.