Wenger kuimarisha ulinzi

Arsenal inaelekea ina mipango ya kuimarisha ulinzi msimu huu, ikiwa itafanikiwa kumsajili mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa, Sebastien Squillaci, kutoka Sevilla ya Uhispania.

Timu ya Sevilla imekubali kwamba imepokea ombi kutoka Arsenal, la kutaka kumsajili kiungo cha kati Squillaci.

Vyombo vya habari vimemnukuu mkurugenzi wa michezo wa Sevilla, Ramon Rodriguez, akizungumza katika uwanja wa ndege mjini Porto.

Arsenal itakuwa na upungufu mkubwa wa wachezaji wa ulinzi, baada ya kuamua kutowaongezea mikataba wachezaji wenye uzoefu mkubwa William Gallas, Sol Campbell na Mikael Silvestre.

Squillaci, mwenye umri wa miaka 30, jana aliitaka timu yake ya Sevilla kutomchagua katika pambano lao dhidi ya Braga ya Ureno, ili baadaye mashindano hayo ya klabu bingwa yasije yakawa kizuizi cha yeye kuondoka.

Mchezaji huyo, ambaye zamani aliimarisha ulinzi wa timu ya Lyon, inakadiriwa hivi sasa ana gharama ya pauni milioni 6.5, lakini bado haijafahamika kikamilifu ikiwa Arsenal watatoa kiasi hicho cha pesa kumpata.

Huku Arsenal ikiwa na mipango ya kumsajili Sebastien, mchezaji wa ulinzi Armand Traore inaelekea ana mipango ya kuelekea Benfica ya Ureno.

Image caption Rory Delap wa Stoke akipambana na Armand Traore wa Arsenal

Mchezaji huyo wa Arsenal, mwenye umri wa miaka 20, aliingia Uingereza baada ya kuihama klabu ya Monaco mwaka 2006.

Lakini hajapata kuichezea Arsenal kikamilifu, na aliazimwa kwa Portsmouth kwa msimu mmoja.

Kutokana na kuwepo pia mchezaji wa kimataifa wa England Kieran Gibbs, inaelekea Traore ameshakamilisha mipango ya kuelekea Ureno.

Benfica imemsajili kwa kutumia pauni milioni 3.2.

Ajenti wa Traore, Richard des Voeux, amesema kwamba "vilabu kadhaa barani Ulaya vilimtaka Armand, lakini uamuzi wa kujiunga na Benfica una manufaa zaidi kwake".