Odemwingie kucheza katika Premier

Klabu ya ligi kuu ya Premier ya England, West Bromwich Albion, leo imefanikiwa kumsajili Peter Odemwingie, kutoka Lokomotiv Moscow ya Urusi.

Image caption Mchezaji wa timu ya taifa ya Nigeria

Odemwingie amekubali mkataba wa miaka miwili.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 ana uraia wa Nigeria, na vile vile Urusi.

Alizaliwa Uzbekistan. Mamake ni Mrusi, na baba ni kutoka Nigeria.

Misimu minne iliyopita amekuwa akiichezea Lokomotiv, na alifanikiwa kufunga magoli 21, na kuwa kati ya wachezaji 11 wanaoanza mechi, mara 70.

Meneja wa West Bromwich Albion, ambayo kwa jina la utani inajulikana kama 'Baggies', Roberto Di Matteo, ameelezea katika tovuti ya klabu kwamba ana furaha mno katika kumkaribisha Peter.

"Ni mchezaji wa kusisimua wa kimataifa, ana CV ya kuvutia, na nina hakika kwamba mchezaji wa kiwango chake kujiunga na klabu ni hatua ambayo itawainua wachezaji wote."

Di Matteo alielezea kwamba mchezaji huyo ana kasi, huitumia miguu yote vizuri, anafunga mabao, na vile vile ana maarifa ya hali ya juu.

"Tumemsajili kama mshambulizi, lakini anaweza kucheza popote, na ananipa nafasi zaidi kuamua acheze wapi", alieleza Di Matteo.

Huyu ni mchezaji wa sita wa kudumu ambaye meneja huyo wa West Brom Albion amemsajili msimu huu.

Wengine waliosajiliwa awali ni Steven Reid, Gabriel Tamas, Pablo Ibanez, Boaz Myhill na Nicky Shorey.