Uganda yawararua Angola

Francisco Zuela
Image caption Kipigo kweli kwa Angola

Uganda iliwathibitishia wageni Angola kwamba inayafahamu maarifa yote katika soka, kwa kuwabwagiza magoli 3-0 mjini Kampala, katika mechi ya kufuzu kushirikishwa katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012.

Mechi hiyo ya Jumamosi ilichezwa katika mazingira ya mvua, na pengine huenda Angola wakatumia kisingizio hicho katika kujitetea.

Kwa mataifa ya Afrika Mashariki, yalikuwa ni matokeo ya kufurahisha mno, kwani awali Tanzania nayo ilikuwa imetoka sare ya 1-1 ugenini Algeria.

Mshambulizi wa Hearts ya Uskochi, David Obua, alimfurahisha sana kocha Bobby Williamson, kwa kuweza kuifanya timu ya Cranes kupata bao la kwanza, kabla ya Andrew Mwesigwa na Geoffrey Sserunkuma kubandika mabao zaidi katika kipindi cha pili.

Wakenya, ambao walifanya vyema katika mechi za kujiandaa, kwa kwenda sare na Tanzania na kupata ushindi Ethiopia, watakuwa ugenini katika mechi nyingine ya kundi J.

Uganda wanajaribu kufuzu kushiriki katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza, tangu walipomaliza nyuma ya Ghana mwaka 1978.

Mara kadhaa Angola waliponea chupuchupu, hadi dakika ya 35, wakati Obua alipotikisa wavu, baada ya pasi safi kutoka kwa Vincent Kayizzi, na kipa Lama hakuona chochote.

Zambia na visiwa vya Comoro iliwabidi kuchelewesha mechi yao ya kundi C mjini Lusaka, angalau kwa saa 24, kutokana na kuchelewa kuwasili kwa mwamuzi na wasaidizi wake.

Morocco nao walikuwa wanapambana na Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mechi ya kundi D.

Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012 yatafanyika katika mataifa ya Gabon na Equatorial Guinea.