TP Mazembe yaibomoa Esperance

Mashabiki wa Mazembe
Image caption Zaidi ya mashabiki 35,000 walitizama mechi katika uwanja wa Kenya

Esperance kutoka Tunisia ilishindwa kucheza kabisa ilipokutana na wenyeji TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, katika mkondo wa kwanza wa fainali mjini Lubumbashi, siku ya Jumapili, na ilifungwa magoli 5-0.

Ushindi huo umeiweka TP Mazembe katika nafasi nzuri ya kuhifadhi ubingwa wake.

Wachezaji Ngandu Kasongo na Given Singuluma, kila mmoja alitia wavuni mabao mawili, na Dioko Kaluyituka akafunga kupitia penalti, na kupunguza kabisa matumaini ya Esperance kunyakua ubingwa katika mechi ya marudiano, itakayochezwa mwezi Novemba.

Esperance walilalamika kwamba bao la kichwa la Ngandu Kasongo halikuvuka msitari baada ya dakika 18 za mchezo, lakini malalamiko yao yalitupiliwa mbali na mwamuzi Mohamed Ben Mansour kutoka Togo.

Mazembe, katika mechi iliyovutia zaidi ya mashabiki 35,000 katika uwanja unaojulikana kwa jina Kenya, waliweza kushangiliwa kikamilifu katika mji huo maarufu kwa shughuli za uchimbaji madini.