Redknapp atisha kuwasusia waandishi

Harry Redknapp
Image caption Amekasirishwa na waandishi habari

Meneja wa klabu ya Tottenham ya England, Harry Redknapp, amesema ataacha kufanya mahojiano na waandishi wa habari, ikiwa ataadhibiwa na chama cha soka cha FA, kwa kuelezea kwamba goli la mchezaji wa Manchester United, Nani, siku ya Jumamosi, lilikuwa ni kichekesho na kashfa.

Chama cha soka FA kitaamua siku ya Jumanne, ikiwa kitamuadhibu Redknapp kwa matamshi hayo, baada ya Man U kuichapa Tottenham magoli 2-0.

"Nawatakia kila la heri iwapo wanataka kuyafanya makuu niliyoyasema, basi hata nami nitazua masuala makuu", alinukuliwa Redknapp.

"Msitazamie mimi kuendelea kujitokeza katika televishini, na kuzungumza na waandishi baada ya mechi, kwani kamwe sitafanya hiyo".

Huku Manchester United ikiongoza kwa bao 1-0, na zikisalia dakika sita kabla ya mechi kumalizika, Nani aliutumbukiza mpira wavuni, baada ya kipa wa Spurs, Heurelho Gomes, kuuweka mpira chini, akidhani alikuwa ameruhusiwa na mwamuzi kupiga free-kick, kufuatia Nani kuunawa mpira.

Lakini wachezaji wa Spurs, na mashabiki wao, walishangazwa na mwamuzi Mark Clattenburg, ambaye aliruhusu bao hilo kuhesabiwa.

Baada ya mechi, Harry Redknapp, kwa kuudhika, alisema "tukio zima lilikuwa ni kichekesho. Aliunawa mpira. Nani aliunawa mpira na maksudi kuushika na kuusukuma chini. Mark Clattenburg ni mwamuzi wa kiwango cha juu, lakini katika hili amekabwa na jinamizi."