England yahofia imeikasirisha FIFA

Kampeni ya England
Image caption David Beckham, Gordon Brown na Wayne Rooney, walipozindua kampeni ya England mwaka 2009

Mjumbe mmoja wa kampeni ya England ya kutaka kupata nafasi ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018, ameelezea kwamba juhudi zao huenda ikawa zimeathiriwa kwa kiasi, kutokana na gazeti moja la Uingereza kuchunguza utaratibu mzima wa nchi kuruhusiwa kuandaa mashindano hayo hufanywa vipi.

Awali, mjumbe mmoja wa kamati kuu ya shirikisho la soka duniani, FIFA, alikuwa amesema habari zilizochapishwa katika gazeti la Sunday Times halitavuruga kwa njia yoyote ile kampeni ya England kuandaa mashindano hayo.

Lakini inaelekea sasa juhudi za Sunday Times kuwachunguza wajumbe wawili wa kamati ya FIFA kumeiacha England ikiwa na kazi kubwa ya kuimarisha uhusiano, kabla shirikisho hilo kuitangaza nchi itakayoandaa mashindano ya mwaka 2018, tarehe 2 Desemba.

"Uchunguzi huo kwa kiasi kikubwa umeathiri ombi la England", afisa mmoja mkuu wa kampeni ya England aliielezea BBC.

Huku zikiwa zimesalia wiki nne kabla ya England kufanya uamuzi, England haijatupilia mbali matumaini ya kuimarisha uhusiano tena kati yake na FIFA.

Maafisa wakuu katika kampeni ya England wameelezea kwamba mipango ya vyombo vya habari kuendelea kuwachunguza maafisa wa FIFA, ikiwa ni pamoja na kipindi cha televisheni cha BBC cha Panorama, huenda yakaiharibia nchi juhudi za kuchaguliwa mwenyeji wa michuano hiyo.

Mjumbe mmoja wa kampeni ya England ameiambia BBC: "Swali muhimu ni je, tutaweza kujinusuru kutoka hayo? Wajumbe wa FIFA wanahisi kwamba wanasulubiwa na vyombo vya habari vya Uingereza".