Mazembe waifunga Esperance

Mazembe
Image caption wachezaji wa Mazembe wakishangilia ushindi wao

Klabu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, TP Mazembe imejishindia ubingwa wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika kwa mara ya nne.

Hii ni baada ya kusababisha sare ya bao moja na Klabu ya Tunisia, Esperance katika mchuano wa duru ya pili ya fainali kufuatia ushindi wa magoli 5-0 mchuano wa kwanza mjini Lubumbashi.

Esperance ilihitaji miujiza kushinda kwa zaidi ya magoli matano na ingawa ilionyesha nia ya kuyatafuta magoli hayo na ushindi, juhudi zao haizikutosha dhidi ya klabu yenye uzowefu ambayo kwa kipindi kirefu ilipooza mikiki mikiki ya Esperance ikisubiri fursa ya kufunga bao la ugenini na kufuta lile ililofungwa.

Kabla ya mchuano huo kuanza polisi walifanya kazi ya ziada kuzuia ghasia zilizoanzishwa na mashabiki wa Esperance waliorusha chupa za maji uwanjani wakati Timu ya Mazembe ilipokuwa ikiingia uwanjani. Kwa mujibu wa taarifa za polisi, mashabiki kadhaa wamekamatwa.

Harrison Afful, nyota wa Timu ya Taifa ya Ghana aliipatia Esperance bao la kwanza mnamo dakika ya 13 ya kipindi cha kwanza lakini likafutwa kwa bao la Deo Kanda zikisalia dakika 20 za mchezo kumalizika.

Bao la Mazembe lilifuatiwa na ghasia lakini polisi walitumia nguvu ya ziada na kuwaondoa mashabiki wengi nje ya uwanja licha ya kuwa mechi ilikuwa bado inaendelea.

Kufuatia ushindi huu Mazembe inajishindia zawadi ya dollar milioni moja na nusu pamoja na kushiriki Kombe la Dunia la Vilabu nchini Abu Dhabi mwezi ujao.

Mazembe itafungua mashindano hayo kwa pambano dhidi ya Klabu bingwa ya Mexico, Pachuca.