FIFA kuchukuwa hatua wanakamati wake

Kamati inayohusika na nidhamu ya shirikisho linalotawala mpira duniani FIFA inatazamiwa kutangaza kama iwachukulie hatua au la wanachama wa Kamati kuu yake waliotangazwa kuhusika na utayarifu wao kuuza kura zao za kuamua ni nchi gani itaandaa fainali za Kombe la Dunia.

Image caption FIFA kuamua

Raia wa Nigeria Amos Adamu na Reynald Temarii kutoka Tahiti walisimamishwa katika kamati hiyo ili kusubiri upelelezi baada ya gazeti la Sunday Times la Uingereza kuchapisha habari kuhusu siri hiyo.

Kuhusu madai hayo ya rushwa hali inaelekea kuwa mbaya zaidi kwa Adamu kutokana na ushahidi wa gazeti hilo aliomba fedha nyingi za ujenzi wa viwanja zipitie majina ya kampuni ya familia yake.

Naye Temarii amesisitiza nia yake ilikuwa kuimarisha vifaa vya michezo nchini mwake katika visiwa vya Pacific bila faida kwake binafsi.

Endapo watachukuliwa hatua basi hawatoshiriki shughuli ya upigaji kura inayotazamiwa kufanyika tarehe 2 Disemba na nafasi zao zitapigiwa kura kupata mrithi mwezi February mwakani. Huku nyuma kiongozi wa timu ya England inayowania fursa ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 amelishutumu shirika la utangazaji la BBC akisema halina uzalendo kwa mipango yake ya kutangaza uchunguzi wake kuhusu FIFA.

Kipindi cha Televishoni cha Panorama kimepanga kutangaza matokeo ya uchunguzi wake kuhusiana na shughuli za FIFA siku tatu kabla ya kura ya kuamua nchi itakayoandaa fainali hizo.

Kipindi hicho amesema Andy Anson Mkuu wa kamati ya kuwania nafasi ya England kuandaa fainali za mwaka 2018 alisema kitaikosesha nchi fursa ya kuandaa fainali hizo.