Blackburn yampata tajiri mpya

Mashabiki wa Blackburn
Image caption Rovers imenunuliwa na familia kutoka India

Timu inayocheza katika ligi kuu ya Premier ya Blackburn Rovers, sasa imenunuliwa na familia ya Rao kutoka India, kwa pauni milioni 43.

Taasisi iliyoanzishwa na aliyekuwa mmiliki wa klabu, Jack Walker, imeuza hisa zake, asilimia 99.9, kwa kampuni ya Vencky London Ltd.

Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Paul Egerton-Vernon amesema: "Tumefurahi sana kuikabidhi familia ya Rao timu ya Rovers".

"Tumefurahishwa na namna walivyoitamani timu, na mipango na mawazo yao kuhusiana na uwekezaji zaidi, na pia mapenzi yao ya kuendelea kuendeleza kumbukumbu za Jack Walker".

Aliongezea: "Kikamilifu tutaheshimu na kuendeleza msimamo wa Jack Walker, na tutafanya juhudi kusaidia katika usimamizi, ili kuhakikisha Blackburn Rovers itaendelea kuwa ni kati ya vilabu vinavyosimamiwa vyema zaidi katika ligi kuu ya Premier".

"Tumefurahishwa hasa na kuwa mapatano hyo yameungwa mkono kikamilifu na taasisi ya Walker, mwenyekiti wake, na vile vile wasimamizi, na ambao bila shaka wataendelea na mamlaka yao, nasi tutawaunga mkono".

Makubaliano hayo yanaifanya Rovers kuwa timu ya kwanza katika ligi kuu ya Premier itakayomilikiwa na matajiri kutoka India, na ambao wana matumaini kwamba maarifa yao katika biashara ya soko la Asia itaiwezesha timu hiyo ya Lancashire kunawiri zaidi.