Blatter aridhika na hatua ya FIFA

FIFA
Image caption Shirikisho limeunga mkono adhabu iliyotolewa

Rais wa shirikisho la soka duniani, FIFA, Sepp Blatter, amesema "ameridhika" na uchunguzi uliofanywa kuhusiana na madai ya ufisadi, na ambao matokeo yake ilikuwa ni kuwasitisha kazi maafisa sita wakuu.

Lakini alikiri kwamba sio wanachama wote katika shirikisho hilo waliomo katika kamati kuu, ambao wamependezwa na matokeo hayo.

"Uamuzi huu sio kwamba umeungwa mkono kikamilifu na wanachama wote wa kamati kuu", alielezea Blatter.

"Lakini kamati kuu....kama serikali ya FIFA, bila shaka inatekeleza na kuzingatia uamuzi huo".

Mjumbe kutoka Nigeria, Amos Adamu, alipigwa marufuku katika shughuli za soka kwa miaka mitatu, huku Reynald Temarii kutoka Tahiti, naye akipigwa marufuku ya mwaka mmoja, kutokana na madai kwamba waliitisha pesa ili kuipigia kura nchi itakayoandaa mashindano ya Kombe la Dunia.

Madai kuhusu wajumbe hao wawili yalifichuliwa na gazeti moja la Uingereza.

Wote wawili walikuwa ni wajumbe wa kamati kuu ya FIFA, na sasa wamepoteza mamlaka ya kupiga kura katika kuamua ni mataifa yapi yatakuwa wenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022.

Maafisa wengine wanne ambao zamani walikuwa katika kamati kuu, Slim Aloulou wa Tunisia, Amadu Diakite kutoka Mali, Ahongalu Fusimalohi wa Tonga na Ismael Bhamjee kutoka Botswana, pia waliadhibiwa.