Panorama sio kikwazo 2018

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron
Image caption Cameron amesema kipindi cha BBC sio kizuizi kwa kampeni ya England ya 2018

Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, amesema uchunguzi wa waandishi wa kipindi cha televisheni cha BBC, Panorama, kuhusiana na ufisadi katika shirikisho la soka duniani, FIFA, unaudhi, lakini hautaathiri juhudi za England kuchaguliwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka 2018.

Kipindi cha BBC kuhusiana na uchunguzi wa shirikisho linalosimamia soka duniani kinatazamiwa kupeperushwa hewani tarehe 29 Novemba, siku tatu kabla ya kura kuamua nchi itakayopewa nafasi hiyo, tarehe 2 Desemba, mjini Zurich, Uswisi.

"Je, ni jambo la kuudhi kwa Panorama kuandaa kipindi hicho zikiwa zimesalia siku chache tu? Bila shaka jibu ni ndio", Cameron alielezea BBC.

"Lakini ni nchi huru. Nadhani Fifa wataelewa hivyo".

Mkurugenzi mkuu wa kampeni za England mwaka 2018, Andy Anson, alikuwa ameilaumu BBC kwa kukosa 'uzalendo', kwa kupanga kipindi hicho kutangazwa kabla tu ya kura kupigwa.

Kutokana pia na ripoti hivi majuzi katika gazeti la Uingereza la Sunday Times, na ambalo uchunguzi wake wa usimamizi wa soka katika shirikisho la Fifa lilichangia katika maafisa wake wawili kupigwa marufuku, na wengine wanne kusitishwa kazi zao, vyombo vya habari vya Uingereza inaelekea vimekuwa vikivuruga matumaini ya England kuandaa mashindano hayo.

Panorama imeutetea uamuzi wake wa kuandaa mashindano hayo, ikisema kipindi hicho bado kitakuwa hewani, kwa kuzingatia 'maslahi ya umma'.

Msemaji wa BBC ameelezea: "Panorama kina sifa za uandishi unaosifika, ulio huru, na uchunguzi unaofanywa kikamilifu".