Bolton yaishinda Blackburn 2-1

Wachezaji wa Bolton
Image caption Bolton walikuwa wameshindwa kuishinda Blackburn katika uwanja wa nyumbani tangu mwaka 2000

Stuart Holden alifanikiwa kufunga bao katika dakika za mwishomwisho, na Bolton kufanikiwa kuandikisha ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Blackburn, katika mechi ya ligi kuu ya Premier iliyochezwa siku ya Jumapili

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2000 kwa Bolton, ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Reebok, kuweza kuibwaga Blackburn.

Mechi hiyo ilikosa msisimko katika kipindi cha kwanza, hadi wakati mchezaji wa Bolton, Mark Davies, alipoamriwa na mwamuzi kuondoka uwanjani, kwa kumpiga Phil Jones kwa kisigino cha mkono.

Blackburn walifanya juhudi, lakini Fabrice Muamba, wa timu ya Bolton, ndiye aliyekuwa wa kwanza kufunga bao, kupitia mkwaju wa chini kwa chini.

Mame Biram Diouf ilielekea ataiwezesha Blackburn kuondoka angalau na pointi moja, lakini huku mambo yakielekea kuwa ni sare, Holden alivuruga mipango hiyo ya Blackburn.

Kwa meneja wa Blackburn, Sam Allardyce, matokeo hayo yalikuwa ya kusikitisha sana, kwa klabu ambayo aliweza kuiongoza hapo zamani pia, kati ya mwaka 1999 hadi 2007, na timu yake ikiwa sasa katika nafasi ya 13, na haimo salama sana kushukishwa hadhi, kwani imevuka kiwango cha kuteremshwa kwa pointi tano tu.

Wolverhampton 1-0 Birmingham

Image caption Bao la Hunt laiwezesha Wolverhampton kuendelea kuwa imara.

Katika mechi nyingine iliyochezwa sambamba na mechi ya Bolton na Blackburn, Wolverhampton iliweza kuishinda Birmingham bao 1-0.

Bao la Stephen Hunt, ikiwa ni pamoja na Wolves kudumisha rekodi nzuri tangu mwezi Aprili, ilikuwa ni nafasi tosha kwa Wolves kujivunia uchezaji wao.

Mlinda lango wa Birmingham, Ben Foster, awali aliweza kuiokoa timu yake kutoka kwa mikwaju ya David Edwards, Hunt na vilevile Ebanks-Blake.

Nafasi ya wageni Birmingham ya kufunga bao ilipatikana wakati Kevin Phillips alipoupata sawia mpira wa kichwa, lakini akauelekeza mbali na lango.

Lakini kwa jumla, Birmingham haikuonyesha maarifa mengi katika mechi hiyo.