Manchester United kileleni tena

Peter Crouch
Image caption Crouch alikosa nafasi ya kuifungia Tottenham goli

Manchester United iliendelea na rekodi yake nzuri ya kutoshindwa katika mechi yoyote msimu huu, baada ya kucheza jumla ya mechi 21, na vile vile kufanikiwa kurudi kileleni katika ligi kuu ya Premier ya England.

Hii ni baada ya kutofungana na Tottenham.

David Beckham alikuwa katika uwanja wa White Hart Lane, akitizama timu ya Tottenham, anayotazamia kuichezea, lakini licha ya yote yale aliyoyaona uwanjani, timu hiyo haikuweza kufunga bao.

Man U ililazimika kucheza dakika 16 za mwisho pasipo mchezaji wao maarufu kutoka Brazil, Rafael, ambaye mwamuzi alimtolea kadi ya pili ya manjano, kwa kumchezea vibaya Benoit Assou-Ekotto.

Hata hivyo Spurs (Tottenham) walishindwa kuitisha Manchester United, licha ya kucheza wakiwa uwanja wa nyumbani.

Mshambulizi Wayne Rooney bado hajafikia hali yake ya ubora kikamilifu, lakini mara mbili aliweza kuitisha Spurs, na kumfanyisha kazi ngumu mlinda lango Heurelho Gomes mapema katika kipindi cha pili.

Spurs pia walipata nafasi za kufunga mabao kupitia Peter Crouch na Rafael van der Vaart lakini hawakufua dafu.

Hata hivyo meneja wa Man U Sir Alex Ferguson ataridhika kwamba walitoka katika uwanja wa kati ya maadui wao wakubwa zaidi pasipo madhara.

Manchester United inawatangulia wapinzani wao wakubwa zaidi, majirani Manchester City, kutokana na wingi wa magoli, na muhimu zaidi, wakiwa na mechi mbili za akiba, na ambazo wanatumaini kuzitumia vyema na hatimaye kuandikisha ubingwa wao wa ligi ya Premier wa 19.