Liverpool yakataa kumuuza Torres

Fernando Torres Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mwezi Mei mwaka jana ombi la Chelsea kumtaka Torres pia halikufaulu

Klabu ya soka ya Liverpool inayocheza soka katika ligi kuu ya Premier ya England, imetangaza kwamba imelikataa ombi la wapinzani Chelsea kutaka kumnunua mshambulizi Fernando Torres.

Licha ya kwamba Torres, mwenye umri wa miaka 26 hajacheza vyema kadri ya kiwango chake msimu huu, angalau ameweza kuifungia Liverpool magoli tisa, katika mechi 25 alizocheza.

"Chelsea waliwasilisha ombi la kutaka kumsajili Fernando, lakini tumelikataa. Mchezaji huyu si wa kuuzwa", msemaji wa klabu ya Liverpool aliielezea BBC.

Inasemekana Chelsea ilikuwa na nia ya kumnunua kwa kiasi cha pauni milioni 35, hadi 40.

Hii ni mara ya pili kwa Chelsea, klabu ya London, kutaka kumnunua mshambulizi huyo, kwani mwezi Mei mwaka jana ilikuwa na mipango kama hiyo.

Chelsea wamekataa kuelezea zaidi kuhusu habari hizo, lakini huku dirisha la usajili likiwa wazi hadi usiku wa Jumatatu, saa 2300 GMT, klabu huenda bila shaka kikaongeza pesa katika kujaribu kumsajili mshambulizi huyo kutoka Uhispania.

Liverpool hapo awali walikuwa na mipango ya kumsajili mshambulizi kutoka Uruguay, Luis Suarez, anayeichezea Ajax ya Uholanzi.

Ajax imeielezea Liverpool kwamba imewapa hadi Jumamosi, tarehe 29 Januari, kufikia mapatano kuhusu mchezaji huyo.