Everton yaizuia Chelsea kutamba

Salomon Kalou
Image caption Kalou ameiwezesha Chelsea kupata nafasi nyingine ya kujaribu kufuzu kuingia raundi ya tano FA

Bao la Salomon Kalou katika kipindi cha pili kiliiwezesha Chelsea kupata nafasi ya kuialika Everton katika kupambana nayo tena, katika uwanja wa nyumbani wa Stamford Bridge.

Louis Saha alikuwa ameiwezesha Everton kupata bao la kwanza, wakati mlinda lango Petr Cech aliposhindwa kuuzuia mpira huo wa kichwa, katika mechi ya raundi ya nne ya Kombe la FA.

Lakini dakika tano tu baada ya kuingia kama mchezaji wa zamu, Kalou aliweza kusawazisha, alipopiga mkwaji wa kasi kutoka yadi 12.

Manchester United pia ilikuwa imetishwa katika uwanja wa ugenini dhidi ya Southampton wa Mt Mary, lakini hatimaye ilijikakamua na kupata ushindi wa magoli 2-1.

Robert Pires naye aliweza kuisaida timu ya Aston Villa kuingia raundi ya tano ya FA, wakati alipofunga bao lake la kwanza walipokutana na Blackburn, na kuwafunga magoli 3-1.

Mchezaji wa kati Pires aliweza kuisaida Villa kuongoza katika mechi hiyo, kabla ya Nathan Delfounesco kuongezea bao la tatu.

Licha ya vitisho vya awali, Birmingham, ambayo tayari imefuzu kucheza fainali ya Kombe la Carling, baada ya kulemewa 2-0 na Coventry, hatimaye iliweza kuingia raundi ya tano ya Kombe la FA, kwa kuwashinda wapinzani wao magoli 3-2.

Bolton ilishindwa kutumia nafasi ya kuchezea nyumbani katika uwanja wa Reebok kuingia raundi ya tano, na itabidi kupambana tena na Wigan, baada ya mchezo kutokuwa na magoli.