Liverpool yataka milioni 50

Liverpool, klabu ya soka ya ligi kuu ya Premier ya England, huenda ikamuuza mshambulizi Fernando Torres, kabla ya dirisha la usajili kufungwa usikuwa wa Jumatatu.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Liverpool yataka pauni milioni 50 kutoka kwa Chelsea kumuuza Torres

Hayo ni ikiwa klabu kitaafikiana kuhusu kitita cha pauni milioni 50 ambacho Liverpool inahitaji kutoka kwa wapinzani wao katika ligi kuu, Chelsea.

Kulingana na habari kutoka uwanja wa Liverpool wa Anfield, mshambulizi huyo huenda akafika Stamford Bridge, ikiwa Chelsea itatoa pesa taslimu pauni milioni 40, na vile vile kumruhusu Nicholas Anelka kuichezea Liverpool.

Liverpool tayari imekataa pauni milioni 35 kutoka Chelsea, katika juhudi za kumnunua Torres, ambaye ilimsajili kutoka Atletico Madrid mwaka 2007.

Ombi hilo la Chelsea kumtaka mshambulizi huyo wa Uhispania mwenye umri wa miaka 26, lilikataliwa Ijumaa iliyopita.

Liverpool haijafurahishwa na juhudi za dakika za mwishomwisho kabla dirisha la usajili kufungwa, Jumatatu, saa 2300 GMT, na timu inaamini Chelsea imekuwa na nia ya kumfanya mchezaji huyo kuwa na hisia za kuondoka Anfield.

Torres ana masharti ya kuondoka Liverpool katika mkataba wake, na lazima klabu kupokea pauni milioni 50 kabla ya kumuachia aondoke, lakini hayo ni ikiwa klabu kitashindwa kufuzu kwa michuano ya ligi ya klabu bingwa msimu huu.

Kwa hiyo hata ikiwa Chelsea watakuwa tayari kutoa pauni milioni 50, klabu ya Liverpool inaamini inaweza kumsihi Torres asiondoke.