Wakuu wa Olimpiki waitetea West Ham

BBC imepata habari kwamba klabu ya West Ham imepigiwa debe na maafisa wakuu wa Olimpiki kwamba itafaa zaidi kuumiliki uwanja wa London, baada ya mashindano ya mwaka 2012.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Vilabu vya West Ham na Tottenham vinawania uwanja wa Olimpiki

Kampuni ya Olympic Park Legacy (OPLC), ambayo ina jukumu la kuamua ni nani atamiliki uwanja huo baada ya mashindano, imeamua kwamba ombi la klabu ya West Ham ni bora zaidi, katika kuendelea kuhifadhi sehemu ya uwanja inayotumika katika riadha, kinyume na wapinzani wao Tottenham ambao pia wanawania nafasi ya kuumiliki uwanja huo.

Wakurugenzi katika bodi ya OPLC watatakikana kuelezea msimamo wao, na kuunga mkono ombi la 'Hammers', yaani West Ham, kuumiliki uwanja, ifikapo Ijumaa.

Serikali na vile vile Meya wa mji wa London baadaye watatangaza uamuzi wao, lakini wanatazamiwa kuunga mkono pendekezo litakalotolewa na OPLC.

Msemaji wa OPLC amesema: "Ni uvumi mtupu kugusia kwamba uamuzi tayari umeshafanyika".

"Bodi yetu itakutana Ijumaa. Kutakuwa na mapendekezo kutoka kwa maafisa wa OPLC kutoka pande zote mbili, na kura itapigwa kuamua ni ombi la nani linawavutia wengi".

Itakuwa jambo la kushangaza ikiwa mawaziri na Meya Boris Johnson, watapinga mapendekezo ya wakurugenzi wa OPLC, na ambao wametumia muda mwingi katika kipindi cha miezi michache iliyopita, wakikagua maelezo na mipango mbalimbali kutoka kwa vilabu vyote viwili, ikiwa watatangaza uamuzi tofauti katika kipindi cha wiki chache zijazo.

West Ham iko radhi sehemu ya riadha ya uwanja isalie, na kuutumia sio tu kwa michezo, bali pia kwa sherehe mbalimbali.