FIFA yatoa onyo kali kwa Wazimbabwe

Rais wa FIFA Sepp Blatter na katibu mkuu Jerome Valcke
Image caption FIFA kuwachukulia hatua wachezaji wa Zimbabwe waliokiri kupanga matokeo ya mechi

Katibu mkuu wa shirikisho la soka duniani, FIFA, Jerome Valcke, amesema mchezaji yeyote wa Zimbabwe ambaye itathibitishwa alihusika katika njama ya udanganyifu kwa kupanga matokeo ya mechi katika mataifa ya Mashariki ya Mbali, inafaa kabisa asiruhusiwe kucheza soka tena.

Wachezaji kadhaa wa Zimbabwe walikubali kutia saini maelezo na kukiri kwamba walihusika katika njama kati ya mwaka 2008 hadi 2009. Hata hivyo, wachezaji hao wamekuwa bado wakivichezea vilabu vyao nchini Afrika Kusini na vile vile Zimbabwe.

"Ikiwa kuna yeyote aliyekiri kufanya hivyo, haifai kabisa aendelee kucheza tena", Valcke aliielezea BBC.

Wachezaji hao wa kimataifa walikuwa wamekiri kwamba walilipwa ili kupoteza mechi dhidi ya Thailand, Malaysia na Syria.