FA: Kevin Davies aomba msamaha

Nahodha Kevin Davies amewataka radhi mashabiki wa Bolton, baada ya timu yake kufungwa magoli 5-0 na Stoke katika uwanja wa Wembley siku ya Jumapili.

Image caption Nahodha wa Bolton amesikitishwa na matokeo ya Jumapili

Timu ya Davies pia ilishindwa katika nusu fainali ya Kombe la FA mwaka 1998, alipokuwa mchezaji wa Chesterfield.

Baada ya mechi, Davies, mwenye umri wa miaka 34, kupitia tovuti ya mawasiliano ya kijamii ya Twitter, aliandika kwamba binafsi aliona ni jambo la "aibu na la haya mno" kushindwa vibaya kiasi hicho.

"Ninasikitika kwamba baada ya kutushangilia na kulipa pesa nyingi", aliandika katika Twitter, "ninahuzunika na kufedheheka kiasi cha kukosa maneno ya kuelezea", aliwaambia mashabiki.

Bolton, ambao wamo katika nafasi ya nane ya ligi kuu ya Premier ya England, na katika msimu ambao wamekuwa wakifanya vyema, kabla ya mwisho wa nusu ya kwanza walikuwa tayari wamefungwa magoli matatu na Stoke, kupitia juhudi za Matthew Etherington, Robert Huth na Kenwyne Jones, na ilionekana wazi itakuwa vigumu kwa wao kupata ushindi katika mechi hiyo.