Houllier alazwa hospitali

Klabu ya Aston Villa imethibitisha kwamba meneja wao, Gerard Houllier, amelazwa hospitali.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Anatazamiwa kulazwa hospitali kwa siku kadha

Meneja huyo, mwenye umri wa miaka 63, alilazwa hospitalini Birmingham, usiku wa kuamikia Alhamisi.

Mkurugenzi mkuu wa Villa, Paul Faulkner, amezungumza naye na kuelezea kwamba Houllier anaendelea kupata nafuu.

Meneja msaidizi Gary McAllister aliachiwa kibarua cha kuwaongoza wachezaji katika mazoezi ya timu hiyo ya Alhamisi.

Houllier anatazamiwa kulazwa hospitalini kwa siku chache, akikaguliwa zaidi afya yake.

McAllister vile vile atausimamia mchezo wa Jumamosi kati ya klabu na Stoke, katika uwanja wa nyumbani wa Villa Park.

Bw Faulkner alielezea kwamba Houllier alizungumza akiwa na matumani makubwa ya kupata nafuu haraka.

"Vile vile nimepata ujumbe mwingi kutoka kwa mashabiki wanaomtakia apate nafuu haraka, na ningelipenda kuwashukuru kwa ukarimu wao katika kumtaka Gerard kupona haraka", alielezea.

"Ninatazamiwa kumuona mchana huu nikiwa na Gary, na nitampitishia ujumbe wa mashabiki".

Houllier alifanyia upasuaji kufuatia kuugua maradhi ya moyo mwaka 2001, alipokuwa meneja wa Liverpool FC.

Alianza kuifunza timu ya Villa Park mwezi Septemba, baada ya kuondoka Martin O'Neill.