Wenger ataka Mabeki warefu msimu ujao

Msimu wa mwaka 2010/2011 ulimalizika kwa huzuni mkubwa kwa Arsenal. Hii ni klabu ambayo matarajio na matumaini ya meneja wake pamoja na wachezaji yalikuwa makubwa na kuyatiririsha kwa mashabiki kupitia ahadi za mambo mazuri kutarajiwa kutoka kwa kikosi madhubuti.

Lakini baada ya kukosea bila kudhania kuwa wangeshindwa na Birminham City kwenye fainali ya Kombe la Carling, klabu ambayo kabla ya hapo ilikuwa ikibabaisha matokeo katika Ligi kuu.

Tangu hapo Arsenal haikuwa na ile mori iliyokuwa nayo hapo kabla ikipoteza mchuano wa kombe la FA dhidi ya mahasimu wao wakuu Manchester United.

Vivyo hivyo maradhi yakazidi kuikumba klabu hiyo iliyodhibiti nafasi ya pili na kuonekana yenye fursa kuipiku Manchester United kabla ya kudorora na hatimaye kumaliza Ligi katika nafasi ya nne.

Mashabiki wa Arsenal wengi wamepoteza imani yao, licha ya klabu yao kuwa na kikosi chenye vijana wenye vipaji na ambao wameimarika katika misimu michache iliyopita, wanahisi mabadiliko yanastahili yafanyike ikiwa klabu hiyo inataka kupata mafanikio kwa vikombe.

Kwa bahati nzuri, Wenger mwenyewe ameahidi kwa kauli yake kufanya mabadiliko na kuondosha mzigo usiofaa kwenye uwanja wa Emirates.

Image caption Kocha Wenger kusajili

Wakati idadi kubwa ya majina ya wachezaji wa kuvutia imetajwa kua tayari kuelekea kaskazini mwa jiji la London, jina moja lililojitokeza kuhama uwanja wa Emirates ni Mrussi Andrei Arshavin.

Mchezaji mwenyewe amesema kuwa Arsene Wenger amemuahidi kuwa bado anataka asalie Emirates.

Pamoja na hayo Wenger akijibu matakwa ya mashabiki amesema hivi karibuni kwamba tatizo kuu lililoikumba Arsenal ni kuvuja kwa mabeki walioruhusu magoli mengi yawapite. Msimu uliopita Arsenal ilibugia jumla ya mabao 43 na mengi yalitokana na mipira ya kutuliza.

Kwa hiyo suluhisho alilopata ni kuwasaka Mabeki warefu watakaoweza kushindania mipira ya juu.

Wenger anasema kuwa tulifungwa mabao mengi ya kupanga na siyo katika mchezo kama ulivyo, kwa hiyo tunahitaji wachezaji wakubwa kwa umbo na warefu kuliko hawa tulio nao. Tunahitaji nguvu ya kupambana dhidi ya mambo fulani fulani kuliko tulivyoweza msimu huu.

Arsenal imeshirikishwa na majina kadhaa ya wachezaji ambao inaweza kuwasajili ili kuleta ile tofauti ya anga.

Miongoni mwao ni Gary Cahill na Mamadou Sakho, hawa wanatazamiwa kuimarisha safu ya ulinzi.

Ingawaje yote hayo yanategemea ni kiasi gani cha fedha alizonazo Wenger. Imearifiwa kuwa beki aliyetajwa hapa Gary Cahill wa Bolton itabidi kuwa na kitita cha pauni milioni 20 kumngoa. Hapa inaonekana Wenger atapitwa na vilabu vingine kutokana na uwezo.

Ukiangazia Ufaransa, beki wa Paris Saint-Germain, mrefu na ni mwamba ambaye wadadisi wote wa soka wanaonelea huyo ndiye mchezaji ambaye Wenger anahitaji.

Halikadhalika Arsenal inatazamiwa kusajili mshambuliaji wa kutegemewa kumsaidia Robin van Persie ambaye hakosi kujeruhiwa kila msimu.