Terry; ni bora Wilshere hakuchaguliwa

Jack Wilshere
Image caption Hatakuwepo katika michuano ya Ulaya kwa vijana chini ya umri wa miaka 21

John Terry ameunga mkono hatua ya kutomshirikisha Jack Wilshere katika kikosi cha England cha vijana chini ya umri wa miaka 21, na ambacho kitapambana katika michuano ya Ulaya baadaye mwezi huu, ikiwa ni hatua ya kumzuia kuchoka mno kupita kiasi.

Terry, nahodha wa timu ya England, alisema kiungo huyo wa kati wa klabu ya Arsenal ni "sehemu kubwa" ya timu ya taifa, na watamhitaji sana iwapo England itafuzu kwa mashindano ya Euro 2012.

"Ikiwa tuna matumaini ya kucheza michuano ya Euro, nilazima kumtunza", alisema Terry.

"Ni bahati mbaya kwa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 21, lakini Jack yumo katiak daraja tofauti kabisa kwa upande wetu."

Stuart Pearce, meneja wa England wa wachezaji chini ya umri wa miaka 21, alimuacha nje Wilshere alipotangaza kikosi chake kitakachoshiriki katika fainali za UEFA ambazo zitafanyika nchini Denmark kuanzia tarehe 11-25 mwezi Juni.

Meneja huyo, baada ya kupokea taarifa ya kimatibabu kutoka timu ya Gunners (Arsenal), alihofia kijana huyo wa miaka 19 huenda akapata majeraha akiendelea kucheza wakati huu wa msimu ya joto, badala ya kupumzika kama wanavyofanya wachezaji wengi walioshiriki katika mechi nyingi msimu uliokwisha.

Wilshere anatazamiwa sasa kuukamilisha msimu wake kwa kucheza Jumamosi katika pambano la kufuzu la Euro 2012, wakati England itakapoikaribisha Uswisi katika uwanja wa Wembley.