Soka ya Italia yaharibiwa na ufisadi

Serikali ya Italia imetangaza kwamba inaanzisha kitengo cha dharura, ambacho kazi yake itakuwa ni kuchunguza madai ya ufisadi kufuatia malalamiko kwamba hayo yamekita sana katika mchezo wa soka, na ambao ni mchezo unaopendwa sana nchini humo.

Waziri wa masuala ya ndani, Roberto Maroni, amesema maafisa wa polisi, wa serikali na vile vile michezo, watafanya mkutano wao wa kwanza, ili kujua watachukua hatua gani.

Image caption Eto ni kati ya wachezaji maarufu wanaocheza katika ligi ya Italia ya Serie A

Hayo yakiendelea, kumekuwa na madai mapya kwamba kamari inayoendeshwa kwa misingi haramu imekuwa ikifanyika, na vile vile kupangwa kwa matokeo ya mechi nchini Italia, matatizo ambayo huenda yakaenea hadi nchini nyingine duniani.

Kitengo hicho kitawajumuisha wataalamu kutoka vikosi maalum vya polisi, ikiwemo wale wa kuchunguza makundi ya mafia, na vile vile kutoka kwa makundi mawili muhimu sana ya michezo, Kamati ya Italia ya michezo ya Olimpili, na shrikisho la soka la Italia.

Lakini Bw Maroni anatambua kwamba Italia ikiwa peke yake haiwezi kupambana na tatizo la kimataifa la kupanga matokeo ya mechi.

Aliutaka muungano wa Ulaya wa EU kuendeleza juhudi za kupambana na hayo kwa kuvuka mipaka ya Ulaya.

Bw Maroni alikuwa akipambana na kashfa iliyojitokeza hivi majuzi kuhusiana na soka ya Italia, wakati kundi moja la Bologna, nchini Italia, lilijaribu kupanga matokeo ya mechi kwa kushirikiana na kundi lingine nchini Singapore.

Wachunguzi wanaamini kwamba kundi hilo lilijaribu kupanga zaidi ya matokeo ya mechi 30 msimu uliopita, ikiwa ni pamoja na ligi kuu ya Serie A, na kuna hisia kwamba maafisa wa vilabu mbalimbali pia walihusika.

Matukio ya hivi karibuni ni tofauti na kashfa mbaya zaidi iliyowahi kutokea nchini Italia, wakati klabu kikubwa zaidi, Juventus, kiliteremshwa daraja, miaka mitano iliyopita.

Wakati huo, muhimu zaidi ilikuwa ni kuonyesha nguvu, na mamlaka katika Serie A. Kashfa ya sasa hivi inaelekea ni jambo la kawaida tu, na inaelekea, la kujinufaisha kwa kupata pesa kwa haraka.