Sofapaka yataka kuandikisha historia

Sofapaka ya Kenya inaamini inaweza kubadilisha matokeo ya upungufu wa magoli matatu dhidi ya wageni Club Africain kutoka Tunisia siku ya Jumapili, na kuwa timu ya kwanza ya nchi hiyo kufuzu kuingia katika makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wakenya wana imani ya kuishinda Club Africain ya Tunisia uwanja wa nyumbani

Timu hiyo ya Nairobi iliwashangaza wengi katika mechi ya mkondo wa pili dhidi ya Ismailia ya Misri, na inatumaini kwamba Jumapili ina uwezo wa kuishinda Club Africain magoli 3-0 ili kuifanya mechi hiyo ya raundi ya nne kumalizika kwa mikwaju ya penalti.

Ikiwa Watunisia watafanikiwa kupata angalau bao moja katika mechi hiyo ya uwanja wa Nyayo mjini Nairobi, kulingana na sheria ya magoli ya ugenini, hayo yatamaanisha Sofapaka itahitaji kupata jumla ya magoli matano, kibarua ambacho bila shaka kitakuwa ni kigumu mno.

"Tulipoanza, hakuna aliyeamini tunaweza kuendelea hadi tulipofika. Kila hatua tuliyoifikia imekuwa ni ufanisi kwetu", alijisifu kocha Francis Kimanzi, akinukuliwa na shirika la habari la AFP.

"Ni vigumu kuiangusha Club Africain, lakini ni jambo ambalo linawezekana. Watunisia hawatutishi kimaarifa wala kiufundi. Matokeo ya mkondo wa kwanza yanathibitisha hayo."

Nahodha James Situma anakubaliana na kocha wake: "Hakuna kitu ambacho hakiwezekani, na tukiwa na matumaini, tunaweza kupata ushindi kama ule tulioupata dhidi ya Ismailia," alieleza mchezaji huyo ambaye inasemekana anasakwa na timu moja huko Albania.

Huku Sofapaka ikiwakaribisha wachezaji kutoka Tunisia, majirani Simba ya Tanzania watakuwa ni wenyeji wa Daring Club Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, katika mechi ya mkondo wa kwanza, na kutazamiwa kupambana tena wikendi ya tarehe 24-26 Juni.