Steve McClaren kuiongoza Nottingham

Aliyekuwa meneja wa timu ya taifa ya England, Steve McClaren, sasa ataiongoza klabu ya Nottingham Forest kama meneja, baada ya kupata mkataba wa miaka mitatu.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption McClaren zamani aliifundisha Middlesbrough ya Uingereza

McClaren, mwenye umri wa miaka 50, anachukua nafasi ya Billy Davies, ambaye alifutwa kazi siku ya Jumapili na klabu hiyo inayocheza katika mashindano ya Championship.

Mara ya mwisho kama meneja, McClaren aliweza kuifundisha Middlesbrough, na aliwahi pia kutoa mafunzo kwa FC Twente ya Uholanzi, na Wolfsburg ya Ujerumani.

"Steve ana rekodi ya kutoa mafunzo na kukisimamia klabu," alielezea mkurugenzi mkuu wa Nottingham Forest, Mark Arthur.

"Klabu kilichukua hatua za haraka kuzipata huduma zake kwa kuwa ni meneja na kocha wa kiwango cha juu asiyepatikana kwa urahisi".

McClaren atajulishwa rasmi kwa mashabiki katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Alhamisi.

Davies alipoteza kazi yake baada ya mara mbili mfululizo kushindwa kuiwezesha timu hiyo kupandishwa daraja.