Kevin Nolan ajiunga na West Ham

Nahodha wa Newcastle United, Kevin Nolan, amekamilisha utaratibu unaostahili na kujiunga na West Ham, ambako amepata mkataba wa miaka mitano.

Image caption Amepata mkataba kuichezea West Ham iliyoshuka daraja

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, na aliyecheza chini ya meneja Sam Allardyce katika klabu ya Bolton, amejiunga na klabu hiyo ya ligi ya Championship pasipo kujulikano kwa kiwango gani cha fedha.

"Kupata nafasi ya kushirikiana tena na Sam kwa mara nyingine tena ni jambo kubwa kwangu," alielezea Nolan katika wavuti ya West Ham.

"West Ham wameonyesha juhudi katika kunitamani na kuwa na ari ya kuhakikisha nitawachezea."

Awali mashauri na Newcastle yalikwama kutokana na kutoafikiana Nolan atapata mkataba wa miaka mingapi.

"Ninafahamu klabu kilitoa ahadi nzuri kwa Kevin, lakini hawakuelewana kuhusiana na mkataba," meneja wa klabu ya Newcastle, maarufu kwa jina Magpies, Alan Pardew, alilieleza jarida la Shields Gazette.

"Ningelipenda kumshukuru Kevin kwa juhudi zake kama mchezaji na nahodha, tangu nilipochukua mamlaka msimu uliopita.

"Alionyesha kipawa cha uongozi, na ninamtakia kila la heri West Ham. Ni klabu nzuri, na ninahakika atastawi".

Nolan, ambaye anatazamiwa kuwa nahodha katika uwanja wa Upton Park, ametoa ahadi za kuwaridhisha mashabiki wote wa West Ham walionyesha uaminifu wao kwa kumpa mkataba wa miaka mitano.