Wanyama aipenda Celtic

Victor Wanyama, ambaye anawindwa na Celtic ya Uskochi, anasisitiza kwamba atakuwa ni mchezaji wa kwanza kusajiliwa msimu huu wa joto na meneja Neil Lennon wa klabu hiyo, katika makubaliano ya pauni milioni moja.

Kiungo cha kati Wanyama, ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa Kenya, kwa hivi sasa anaichezea timu ya Ubelgiji ya Germinal Beerschot.

Haki miliki ya picha EMPIRIC Sport
Image caption Amesema anaipenda Celtic zaidi kati ya timu zinazomkamia

Mkataba wake unaendelea hadi mwezi Mei mwaka ujao.

Wanyama amevivutia vilabu vya Rangers na Celtic vya Uskochi, Aston Villa inayocheza katika ligi kuu ya Premier ya England, na vilevile timu za Racing Genk na Standard Liege za Ubelgiji.

Lakini Wanyama anasema anakaribia kukamilisha mapatano kuhusiana na masuala ya kibinafsi na klabu ya Celtic, na watu wenye uhusiano wa karibu mno na mchezaji huyo wanaelezea kwamba makubaliano huenda hata yakafanyika katika kipindi cha saa 48 zijazo.

Mbinu za kutumia nguvu za mchezaji huyo, mwenye umri wa miaka 20, zinalinganishwa na Michael Essien, kiungo cha kati katika timu ya Chelsea.

"Nimefurahi sana. Celtic ni klabu yenye historia ya kuvutia, na ninatazamia kuwa nao.

"Nimefurahia kuwa na GBA (Germinal Beerschot Antwerp) na ninatazamia ukurasa mpya katika kuichezea Celtic."

Wanyama, ambaye ni ndugu na mchezaji wa Inter Milan, McDonald Mariga, kwa mara ya kwanza alishiriki katika mechi ya kimataifa akiwa na umri wa miaka 15.

Ilikuwa ni mechi ya kirafiki kati ya Kenya na Nigeria miaka mitano iliyopita.

Meneja wa Celtic, Lennon, ambaye amekuwa akitaka kumsajili Wanyama, tayari amewasajili wachezaji wawili kabla ya ligi ya Uskochi kuanza; mchezaji wa ulinzi Adam Matthews aliyekuwa akiichezea Cardiff City na mlinzi wa Nottingham Forest, Kelvin Wilson.

Wachezaji hao wote wawili walitia saini makubaliano ya awali tangu mwezi Januari.