Hatma ya Bin Hammam Fifa kufichuliwa

Kamati ya Fifa inayohusika na maadili itakutana kesho July 22 na jumamosi tarehe 23 kusikiliza kesi dhidi ya Mohamed bin Hammam, aliyesimamishwa uwanachama kufuatia madai ya rushwa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Makao ya FIFA

Mohamed Bin Hammam anakabiliwa na tuhuma za ufisadi, ikiwa ni pamoja na madai kwamba alinunua kura zilizoiwezesha Qatar kushinda kuandaa fainali ya Kombe la Dunia ya mwaka 2022.

Upelelezi umemalizika na ripoti imetumwa kwa Rais wa shirikisho la Bara Asia aliyesimamishwa Bin Hammam.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bin Hammam

Kizimbani pia watakuemo Maofisa wa Chama cha mpira cha Caribbean Debbie Minguell na Jason Sylvester ambao kesi zao zitasikilizwa pia.

Minguell na Sylvester walisimamishwa pamoja na makamu wa Rais wa Fifa Jack Warner, ambaye upelelezi juu yake ulisimamishwa baada ya mwenyewe kujiuzulu kutoka shughuli zote za mpira.

Tuhuma hizo zinahusiana na mkutano wa vyama 25 vya soka kutoka eneo la Caribian mnamo mwezi May ambapo inadaiwa kuwa hongo ya hadi dola $40,000 zilitolewa na Bin Hammam kwa kila mjumbe wakati akifanya kampeni za kutaka achaguliwe kuwa Rais wa Fifa.

"mnamo tarehe 23 July, kamati ya maadili itajadili na kuchukuwa uwamuzi juu ya kesi zote hizo."

Matokeo ya uchunguzi huo yatakuwa kigezo kikubwa kwa Sepp Blatter kuhusiana na ahadi aliyotoa ya kusafisha shirika hilo lililochafuka kutokana na madai ya ufisadi.

Ingawaje Bin Hammam amekanusha madai ya kuwa alihonga wajumbe wa Fifa inakisiwa kuwa atafungiwa kutoshiriki masuala yote yanayogusa soka baada ya kikao cha ijumaa mjini Zurich

Hta hivyo matokeo barani Afrika yamezua masuali juu ya uwezo wa shirika la Fifa wa kuidhinisha amri zake dhidi ya maofisa wawili waliokiuka maadili wanayotakiwa kutimiza.

Wanachama wa zamani wa Fifa Slim Aloulou wa Tunisia,na Amadou Diakite wa Mali walisimamishwa baada ya tuhuma kuwa walipokea milungula ili waipigie kura Morocco kuandaa fainali ya Kombe la Dunia la mwaka 2010.

Aloulou alipigwa marufuku kutoshiriki shughuli za soka kwa miaka miwili wakati Diakite alifungiwa miaka mitatu. Wote baadaye walipunguziwa adhabu kufikia mwaka mmoja kufuatia rufaa walioyowasilisha mwezi Febuari.

Licha ya adhabu hizi shirikisho la kandanda barani Afrika, CAF limewaorodhesha kwenye kamati kadhaa kwa kipindi cha mwaka 2011 hadi mwaka 2013.

Habari hizi ziliandikwa na mwandishi wa habari wa gazeti la Nigeria Osasu Obayiuwana.

Image caption CAF imepuuza Fifa

Kufuatia ufichuzi huo Fifa inasema imelitaka shirika la CAF lifafanue kuhusu madai hayo.

"Fifa limelitaka CAF lihakikishe kuwa wakati wote wa kipindi cha marufuku kwa maofisa hao, majina ya Slim Aloulou pamoja na Amadou Diakite hayatangazwi kuwa kwenye Kamati za CAF vinginevyo majina hayo yabandikwe kuwa hawaruhusiwi kushiriki shughuli za soka.

Hata hivyo inashangaza kuona kuwa Caf imewatumia il hali kiwango cha kesi yao na marufuku iliyofuata, ni jambo lililotangazwa mno. Je, licha ya amri ya Fifa, ikiwa majina hayo yatazidi kuwekwa kwenye vikao vya kamati za Caf, Fifa itafanya nini?

Kwa mujibu wa taarifa zilizovuja kuhusu kesi ya Bin Hammam, iliyoongozwa na Mkurugenzi wa zamani wa shirika la kijasusi huko Marekani, FBI Louis Freeh, hakuna ushahidi wowote unaomhusisha Bin Hammam na kitendo cha kuwahonga maofisa wa chama cha mpira cha Carribean.

Lakini hisia ndani ya FIFA ni kwamba ushahidi walio nao ni mzito kiasi kwamba Bin Hammam atafungiwa asishiriki shughuli zote za soka.

Kwa hiyo Bin Hammam atafika mbele ya Kamati au atakipiga chenga kikao, akijiwapa fursa zaidi ya kumchukulia hatua au atawaachia mawakili wake wamtetee na kuomba rufaa katika koti za Uswizi?

Blatter anafahamu vyema kua huu ni wakati wa kutakasa jina lake binafsi na la Fifa na siyo wakati wa kuonyesha kuwa kamati ya maadili ni chombo kisicho meno.