Sweden yaishinda Ufaransa 2-1

Siku ya Jumamosi Sweden iliweza kuishinda Ufaransa magoli 2-1, na kumaliza katika nafasi ya tatu ya mashindano ya Kombe la Dunia kwa kina dada nchini Ujerumani.

Mchezaji wa zamu Marie Hammarstrom alipata bao la ushindi dakika za mwishomwisho.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Sweden imeshikilia nafasi ya tatu katika Kombe la Dunia kwa kina dada

Mchezaji huyo aliweza kuupata mpira kufuatia juhudi hafifu za Ufaransa kuuondoa mpira wa kona hatarini, na mchezaji huyo aliweza vilevile kuwaepuka kwa urahisi wapinzani Eugenie Le Sommer na Sonia Bompastor.

Sweden ndio iliyokuwa ya kwanza kutangulia kupata bao katika mechi hiyo.

Kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza, Sweden ilikuwa inaongoza bao 1-0, bao ambalo lilikuwa limefungwa na mshambulizi Lotta Schelin, katika dakika ya 29 ya mchezo.

Lakini katika kipindi cha pili, Mfaransa Elodie Thomis aliweza kufunga bao la kusawazisha katika dakika ya 56.

Jumapili fainali itachezwa, wakati Japan itapambana na Marekani mjini Frankfurt.

Mechi hiyo itaanza saa nne kasorobo usiku kwa saa za Afrika Mashariki.