Man City yakubali kumuuza Tevez

Meneja wa klabu ya Manchester City, Roberto Mancini, amesema makubaliano yameafikiwa na klabu ya Corinthians ya Brazil, kumhusu mshambulizi kutoka Argentina, Carlos Tevez.

Wiki iliyopita, ahadi za Corinthians kumnunua kwa pauni milioni 39 zilitupiliwa mbali na City, na inaaminika klabu kinataka kumuuza kwa pauni milioni 50.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Anataka kuikaribia zaidi familia yake nchini Argentina

Tevez, mwenye umri wa miaka 27, amesema angelipenda kutoka ligi kuu ya Premier ya England, ili awe karibu zaidi na familia yake nchini Argentina.

"Tuna makubaliano na Corinthians, lakini Carlos bado ni mchezaji wa City", Mancini alilielezea alipozungumza katika matangazo ya televisheni ya Sky Sports.

Klabu hiyo ya Sao Paulo, nchini Brazil, na huku ikiwa ndio tu imefanya makubaliano ya kupata fedha zaidi kutoka televisheni, ina juhudi za kumsajili Tevez na kumrudisha katika klabu ambayo aliweza kusifika kama mchezaji mahiri, na akipata ufanisi mkubwa.

Kurudi Marekani ya Kusini pia kutamsaidia Tevez kuwakaribia watoto wake wawili.