Wenger asifu moyo wa vijana

Meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amewasifu vijana wake kwa kumuondolea mashaka na wasiwasi uliotanda na kuikumba klabu hiyo katika majuma ya hivi karibuni kwa kuiondoa klabu ya Utaliano Udinese na hivyo kujipatia tiketi ya kushiriki michuano ya hatua za Ligi ya mabingwa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Arsenal ikitifuana na Udinese ya Italia

Alikuwa nahodha Robin van Persie aliyerudisha bao la Antonio di Natale alipofuta bao la Arsenal lililofungwa na Theo Walcott katika mechi ya kwanza kwenye uwanja wa Emirates wiki iliyopita na hivyo kutimiza ushindi wa 2-1 na jumla ya 3-1.

Baada ya mechi hiyo Wenger akasema kuwa 'bila shaka ni afuweni kwa sababu hatukutaka kuondolewa mapema"

Hili limedhihirisha kuwa hata tuna uwezo wa kusahau matatizo yetu na kujibu kwa kucheza soka yetu kama tunavyocheza kawaida yetu.

Klabu ya Arsenal imehimili kipindi kigumu ikiwa ni pamoja na kuwapoteza wachezaji wake nyota, ambapo Cesc Fabregas alihamia klabu ya Barcelona na Samir Nasri kujiunga na Manchester City.

Katika mechi yao ya kuanza msimu wa Ligi kuu ya England Arsenal ilitoka sare ya 0-0 ugenini dhidi ya Newcastle na kuchapwa na Liverpool nyumbani bao 2-0 uwanja wa Emirates jumapili iliyopita.

Ushindi wa Arsenal dhidi ya Udinese ni afuweni kubwa kwani ingekuwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 14 klabu hiyo kukosa kushiriki Ligi kuu ya vilabu barani Ulaya na hivyo kupoteza angalau zawadi ya pauni milioni 20 za kufikia hatua ya makundi.

Kuhusu uwezekano wa kusajili wachezaji wapya kabla ya soko la usajili kufungwa tarehe 31 agosti, Wenger alijibu tunajitahidi, bila kutoa maelezo zaidi.

Alidokezea tu kwa kusema huenda tukasajili lakini siwezi kutaja majina. Sitoweza kuahidi kuwa tutamsajili fulani kesho.