Kenny Dalglish amtetea Andy Carroll

Fabio Capello na Andy Carroll
Image caption Meneja wa England amemtaka Carroll kurekebisha maisha yake kwa kupunguza ulevi

Meneja wa klabu ya soka ya Liverpool, Kenny Dalglish, amemtetea mchezaji Andy Carroll, kufuatia madai ya kocha wa timu ya taifa ya England, Fabio Capello, kuhusu starehe za kibinafsi za mchezaji huyo.

Carroll alikuwa ni mchezaji wa zamu katika mechi ambayo England ilipata ushindi ilipocheza dhidi ya Wales.

Capello awali alikuwa amesema: "Ikiwa anataka kuwa mchezaji mzuri, basi ni lazima apunguze kinywaji zaidi wa wenzake".

Lakini Dalglish amesisitiza: "Hali yake ya afya ni bora zaidi kumshinda yeyote yule.

"Sidhani maisha na starehe zake za kibinafsi sio kama inavyofikiriwa katika kutafuta cha kuandika kumhusu".

Meneja wa Liverpool aliongezea: "Andy hakuwa katika hali nzuri msimu uliopita kutokana na jeraha la goti.

"Tunafurahia hali yake ya afya msimu huu kwa kwa jeraha hilo limetoweka".

Carroll, mwenye umri wa miaka 22, amecheza tangu mwanzo katika mechi mbili, kati ya mechi nne za Liverpool, tangu alipofika katika uwanja wa Anfield, kufuatia kuhama kutoka Newcastle mwezi Januari.

Mchezaji huyo alifunga mara moja katika pambano la Kombe la Carling dhidi ya Exeter, lakini msimu uliopita, aliweza kutumbukiza magoli mawili katika lango la Manchester City, wakati timu yake ilipopata ushindi wa magoli 3-0.

Dalglish aliongeza: "Nadhani Andy anapokea mawaidha vyema hasa kutoka kwa yeyote yule mwenye uzoefu katika mchezo wa soka".

"Nadhani amepokea vyema mawaidha ya Capello kwa kuwa anamheshimu sana, na nadhani, Fabio Capello naye amheshimu sana Andy Carroll".