Teves asimamishwa na Man City.

Haki miliki ya picha Getty Images

Manchester City imemsimamisha mwamba wao Carlos Tevez kufuatia madai kwamba aligoma kuingia uwanjani kucheza katika mpambano ambao walifungwa 2-0 na Bayern Munich.

Tevez, mwenye umri wa miaka 27, ambaye anasema ugomvi wa sasa ulitokana na kushindwa kuelewana na Meneja wake Roberto Mancini amesimamishwa kuichezea timu ya Manchester City kwa wiki mbili, huku Klabu hicho kikianzisha uchunguzi.

"Kusimamishwa kwa mchezaji huyo kutatoa fursa ya uchunguzi kamili kufanyika kutokana na madai ya utovu wake wa nidhamu", taarifa kutoka Man City imesema.

"Katika kipindi hicho mchezaji huyo hatajumuishwa katika mechi za Klabu hiyo au hata mazoezi yake".

Katika mechi yao na Beryan Munich, Meneja Roberto Mancini alitaka kumuingiza Tevez uwanjani kuchukuwa mahali pa Samir Nasri ili kuiokoa Man City ambayo wakati huo ilikuwa imelala 2-0.

Lakini mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina alionekana kugoma kuingia uwanjani na baadaye Mancini alisema " alikataa kuingia uwanjani. Nilichomuambia Carlos ni kati yangu , yeye na timu. Nimekasirishwa sana kwa sababu ni Carlos, mimi ndiye mwenye uwezo wa kuwabadilisha wachezaji.

" Laiti ningeliruhusiwa , angelikuwa nje. Mimi na yeye tumemalizana.

"Sisi kama timu ikiwa tunataka kuimarika , Carlos hawezi kuichezea timu yetu. Kwa upande wangu, amekwisha"

Siku ya Jumatano asubuhi ,Tevez alitoa taarifa akisema " huu sio wakati wa kuanza kudadisi kwa nini jambo fulani halikufanyika".

"Tukisonga mbele niko tayari kurudi uwanjani na kuichezea Man City ili nitimize wajibu wangu, ikiwa nitahitajika".

Na idhaa ya BBC michezo imefahamishwa kuwa Carlos Teves ambaye zamani ilikuwa mchezaji wa West Ham na Manchester United hakufurahishwa na jinsi maelezo yake kuhusu kilicho tokea yalivyoelezwa.