Arsenal yafungwa licha ya kung'ara

Wachezaji wa Arsenal Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wengi wanaamini Arsenal ilicheza vyema Jumapili licha ya kufungwa na Tottenham

Bao la Kyle Walker kutoka yadi 25 liliiwezesha Tottenham kupata ushindi katika uwanja wa nyumbani White Hart Lane, dhidi ya wageni Arsenal, katika mechi ya kusisimua sana kaskazini mwa mji wa London.

Mlinzi Walker aliweza kufunga bao hilo katika dakika ya 73.

Bao la kwanza la mechi hiyo la Tottenham lilifungwa na Rafael van der Vaart katika kipindi cha kwanza, baada ya kuupokea mpira kutoka kwa Emmanuel Adebayor.

Aaron Ramsey aliweza kusawazisha katika kipindi cha pili, baada ya kupata mpira kutoka kwa Alex Song.

Ingawa Wojciech Szczesny angeliweza kuokoa mkwaju wa Walker, ni lazima ikumbukwe kwamba aliweza kuzima mikwaju ya Adebayor na Jermain Defoe.

Gareth Bale bale alikuwa pia na nafasi ya kuiwezesha Spurs kufunga mkwaju wa tatu, lakini juhudi zake ziliangukia patupu.

Katika mechi nyingine zilizochezwa awali Jumapili, Bolton ikichezea nyumbani uwanja wa Reebok ilifungwa na wageni Chelsea magoli 5-1.

Swansea nayo inaweza kujivunia ushindi baada ya kuwakaribisha Stoke na kuwafunga magoli 2-0.

Lakini hakuna timu ambayo imethibitisha ugumu wa ligi kuu ya Premier kama QPR, kwani walipoitembelea Fulham, walizabwa magoli 6-0, na kuondoka pasipo hata kupata moja la kufutia machozi.