BBC Swahili

Mwanzo > Michezo

Ethiopia, Kenya zang'ara mita elfu kumi

Facebook Twitter Google+
4 Agosti 2012 14:40
Dibaba Tirunesh wa Ethiopia dhahabu mbio za mita elfu kumi wanawake London Olympics

Dibaba Tirunesh wa Ethiopia ameibuka wa kwanza kwa kupata medali ya dhahabu katika fainali za mashindano ya mbio za mita elfu kumi kwa wanawake. Dibaba alimaliza mbio hizo katika dakika 30 sekunde 20 nukta 75.

Naye Yego Sally Jepkosgei kutoka kenya alishika nafasi ya pili na kupata medali ya fedha akitumia dakika 30 sekunde 26 nukta 37, huku Vivian Cheruiyot Jepkemoi naye kutoka Kenya akishika nafasi ya tatu na kupata medali ya shaba baada ya kutumia dakika 30 sekunde 30 nukta 44 .

Sally anasema licha ya Kenya kutokupata medali ya dhahabu lakini kwao ni mwanzo mzuri kupata mafanikio hayo katika London Olympics.

Akizungumza na BBC Swahili baada ya mbio hizo Vivian aliyekuwa akipewa kipaumbele kumdhibiti Muithopia Tirunesh, anasema hakufurahia sana matokeo yake licha ya kupata medali ya shaba kwani alitarajia kufanya vizuri zaidi. ''Sijafurahia vile nilivyofanya lakini shindano lilikuwa ni zuri, lakini wakati wa hatua ya mwisho sikukimbia namna ambayo hukimbia, nilikuwa nimechoka kidogo.'' Anasema

Mwaka 2008 katika mashindano ya michezo ya Olympic jijini Beijing, Kenya haikuweza kufanikiwa kupata medali katika mashindano hayo upande wa wanawake mbio za mita elfu kumi.

Vivian na Sally Jepkosgei wanatarajiwa pia wanatarajia kushiriki mashindano ya mbio za mita elfu tano kwa wanawake jijini London.

Naye Joyce Kirui aliondoka katika mashindano hayo ikiwa imebaki raundi sita baada ya kujeruhiwa wakati wa mashindano hayo jijini London.

Katika mbio za mchujo wa nusu fainali mbio za mita elfu moja mia tano kwa upande wa wanaume waliofuzu ni Kiplagat na Asbel Kiprop.

Awali timu ya Kenya ilifanikiwa kukata rufaa katika shindano hilo baada ya Nickson Chepseba kutegwa wakati akikimbia kulikosababisha amalize nje ya waliofuzu. Baada ya rufaa hiyo sasa atashiriki mashindano ya nusu fainali siku ya Jumapili.

Wengine waliofuzu ni Taoufik Makhloufi kutoka Algeria , Mohamed Moustaoui kutoka Morocco, Mekonnen Gebremedhin kutoka Ethiopia na Abdalaati Iguider kutoka Morocco.

Alamisha hii

Email Facebook Google+ Twitter