Al Shabaab yaburuta miili ya wanajeshi

Taarifa kutoka Somalia zinasema kwamba kundi la kigaidi la Al-shabaab limeonyesha hadharani miili ya wanajeshi linalodai kuwa ni wa kikosi cha kudumisha amani cha Muungano wa Afrika (AU), waliouawa katika mapigano makali mjini Mogadishu.

Walioshuhudia wanasema walihesabu takriban miili sitini baadhi yao ikiwa inaburutwa na watu waliokuwa na hamaki.

Hata hivyo miili hiyo haijatambuliwa rasmi.

Muungano wa afrika umeripotiwa kusema kuwa wanajeshi wake kumi wameuawa mjini Mogadishu huku mapigano yakiendelea hadi usiku wa kuamkia leo.

Wanajeshi wa AU wamekuwa wakivamia maeneo yaliyosalia chini ya utawala wa kundi hilo la kigaidi mjini Mogadishu.