Feri yashika moto kwenye bahari ya Shamu

Takriban watu 800 wengi wao wakiwa ni raia wa Misri wameokolewa kutoka feri iliyoshika moto katika Bahari ya Shamu. Wengine 400 bado wamekwama katika Feri hiyo.

Feri hiyo ilikuwa imetoka katika bandari ya Aqaba nchini Jordan, ikielekea katika bandari ya Nuweiba iliyoko katika Bahari ya Shamu nchini Misri.

Ripoti zinasema kuwa feri hiyo ilikuwa na zaidi ya abiria 1200 wengi wao raia wa Misri.

Maafisa wanaosimamia safari za meli wanasema feri hiyo ilishika moto muda mfupi baada ya kuondoka bandari ya Aqaba. Moto huo unaaminika kuanza katika eneo la kuegeshea magari.

Zaidi ya watu 800 waliokolewa kupitia vifaa maalum na kusafirishwa kwa mashua ndogo. Kwa sasa wamepelekwa katika bandari ya Nuweiba.