Ugiriki: Papandreou 'huenda akajiuzulu'

Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou, amekuwa akifanya mkutano wa dharura na baraza la mawaziri wa nchi hiyo, huku kukiwa na ripoti zinazopingana kuhusu hatma ya utawala wake.

Shaka kuhusu utawala wake inafuatia mpango wake uliozusha mabishano makali wa kutaka kuwepo kwa kura ya maoni kuhusu mpango wa hivi karibuni wa kuunusuru uchumi wa nchi hiyo, alioutangaza mapema wiki hii.

Baadhi wanasema Bwana Papendreou anajiandaa kujiuzulu kama inavyopendekezwa na upinzani, lakini ripoti zingine zinasema kwamba amejitolea kubakia madarakani.

Bwana Papandreou anatarajiwa kulihutubia bunge baadaye leo.

Hatua hii ya sasa inajiri baada ya mawaziri wanne na baadhi ya wabunge kusema hawaungi mkono mpango wa Bwana Papandreou wa kuitisha kura ya maoni.