Rwanda kurejeshea DRC madini yake

Serikali ya Rwanda inatarajiwa kurejeshea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo madini yake, yaliyopatikana magharibi mwa Rwanda katika maeneo ya Rusizi na Rubavu baada ya kuingizwa Rwanda kwa njia za magendo.

Madini hayo yalipatikana miezi mitano iliyopita na yana uzito wa tani 82. Madini yaliyokamatwa ni pamoja na yale ya chuma na bati.

Yalinaswa na maafisa wa ulinzi katika harakati za kupambana na biashara haramu ya madini.

Hafla ya kuikabidhi DRC madini yake itafanyika mjini Rubavu karibu na mji wa Goma, kwenye mpaka baina ya nchi hizo mbili.