Makampuni ya migodi Zambia yashutumiwa

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeshtumu makampuni ya uchimbaji migodi kutoka Uchina yaliyoko nchini Zambia, kwa kuendesha shughuli zake kwa njia isiyokuwa salama na kukiuka haki za wafanyakazi.

Shirika hilo limesema kuwa wafanyakazi katika makampuni manne yanayomilikiwa na Wachina wameelezea kuwa wao hulazimishwa kufanya kazi katika migodi iliyojaa mvuke.

Wafanyakazi hao pia wanadai kuwa wao hulazimika kununua vifaa vyao vya usalama.

Mbali na hayo, wamiliki wa makampuni hayo ya migodi wanadaiwa kuwatisha wafanyakazi wake kuwa watawafukuza kazi iwapo watajiunga na vyama vya wafanyakazi.

Shirika la Human Rights Watch linatoa wito kwa rais wa Zambia Michael Sata kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa uchaguzi wa urais na kuchukua hatua kali dhidi ya makampuni hayo.