Hospitali Syria yapokea maiti zaidi

Maafisa wa Afya nchini Syria wameiambia BBC kwamba hospitali ya kitaifa katika mji wa Homs imepokea zaidi ya maiti 100 katika kipindi cha saa 48 zilizopita. Watu wasiopungua ishirini waliripotiwa kufariki dunia katika mji huo jana Alhamisi, na ripoti zinaashiria kwamba watu wawili waliuwawa kwa kupigwa risasi leo asubuhi.

Karibu na mji wa kusini wa Deraa, shirika la kutetea haki za kibinaadamu la Syrian Observatory for Human Rights limesema kwamba raia wawili wa taifa hilo waliuwawa kwa kupigwa risasi wakijaribu kutorokea nchini Jordan.

Kumetokea maandamano ya kuipinga serikali katika vitongoji mbali mbali vya mji mkuu wa Damascus na pia mji wa kaskazini wa Qamishly.

Mapema juma hili muungano wa mataifa ya kiarabu ulisema kuwa Syria ilikuwa imekubaliana na mpango wa kusitisha ghasia za kisiasa na kuondoa vikosi vyake barabarani pamoja na kuanzisha mazungumzo yakayoleta maridhiano ya kitaifa katika kipindi cha majuma mawili.