Hatma ya Berlusconi kujulikana bungeni

Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi, anakabiliwa na kura muhimu bungeni hii leo wakati nchi hiyo ikijitahidi kuepuka kuangukia kwenye msukosuko wa kiuchumi unaotishia nchi zinazotumia sarafu ya Euro.

Kura hii kuhusu bajeti ya nchi itabainisha ikiwa serikali imepoteza umaarufu wake bungeni.

Hata hivyo Bw Berlusconi anasema serikali yake inaungwa mkono kwa kiasi kinachohitajika. Hofu ni kuwa akishindwa, wabunge wa upinzani wataitisha kura ya kutokuwa na imani naye.

Changamoto inayomkabili Waziri mkuu Berlusconi, ni msukumo kutoka wawekezaji kwenye masoko ya fedha duniani ambao kwa sasa hawana imani kuwa anaweza kutatua matatizo yanayokabili uchumi wa Italia.