Waziri aaga dunia kwenye ajali ya ndege

Rais wa Mexico, Felipe Calderon, amefutilia mbali ziara yake nchini marekani kuhudhuria mkutano wa viongozi wa serikali wa mataifa ya kanda ya Asia na Pacifi mjini Hawii wikendi hii, kufuatia kifo cha waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo, Francisco Blake Mora, kufuatia ajali ya ndege.

Blake alikuwa mmoja wa washirika wa karibu wa rais Calderon, na alihusika moja kwa moja na mikakati ya kupambana na walanguzi wa mihadarati nchini Mexico.

Rais Calderon amesema ajali hiyo ya ndege iliyotokea mjini Mexico city ilisababishwa na hali mbaya ya anga, lakini amehaidi kuwa uchunguzi kamili utafanyika.

Watu wote wanane waliokuwa kwenye ndege hiyo waliaga dunia.

Kifo cha Blake kimejiri miaka mitatu baada ya mtangulizi wake Juan Camilo Mourino, kuuawa kwenye ajali ya ndege.