Maambukizi ya HIV yapungua duniani

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na maradhi ya ukimwi, UN-AIDS linasema kuwa maambukizi ya virusi vya HIV yamepungua kwa asilimia ishirini.

Hiki ni kiwango cha chini zaidi kushuhudiwa katika miaka kumi na minne iliyopita.

Hata hivyo katika bara Afrika viwango hivyo vimesalia kuwa juu. Afrika Kusini ambayo ina wagonjwa milioni tano nukta sita wenye virusi vya HIV inaongoza kwa visa hivi Afrika.

Katika ripoti yake ya kila mwaka shirika hilo linasema jitihada za kimataifa katika miaka kumi iliyopita zimesaidia pakubwa kupunguza maambukizi hayo.

Idadi ya watu wanaofariki dunia kutokana na maradhi yanayosababishwa na Ukimwi pia imepungua kutokana na kupatikana kwa urahisi kwa matibabu.