Machafuko mapya yatokea nchini Misri

Mapigano makali yamekuwa yakiendelea nchini Misri baina ya polisi na waandamanaji katika mji mkuu Cairo.

Kitovu cha machafuko hayo ni eneo la Tahrir karibu na wizara ya masuala ya ndani ya nchi.

Watu kumi na watatu wameuawa katika kipindi cha siku mbili katika ghasia hizi.

Polisi wametumia risasi za plastiki, gesi ya kutoa machozi na virungu kuwatawanya waandamanaji walio na hasira kuhusu namna jeshi linavyoongoza nchi hiyo baada ya kupinduliwa kwa Hosni Mubarak mwezi Februari. Wanamtaka kiongozi wa jeshi kuachia ngazi.

Machafuko haya yamegubika uchaguzi wa wabunge uliopangwa kufanyika wiki ijayo, ukiwa ndio wa kwanza tangu mapinduzi ya Mubarak.