Sudan yavutana kuhusu mafuta na Kusini

Serikali ya Sudan imezuia uuzaji wa mafuta kutoka Sudan Kusini katika mgogoro juu ya ada inayotakiwa kutolewa ili kupitishia bidhaa hiyo nchini humo.

Waziri wa mafuta wa Sudan, Ali Ahmed Osman, alisema upande wa kusini unadaiwa takriban dola milioni 370.

Kiwango hicho ni madeni ya tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwezi Julai.

Suala hilo la ada ni lenye ubishani mzito ambalo halijapata ufumbuzi baina ya nchi hizo mbili.

Nchi zote mbili zinategemea sana mapato ya mafuta kutokana na mauzo yake nchi za nje.