Raia nchini Gambia kumchagua Rais

Raia wa Gambia leo wanashriki katika uchaguzi wa rais ambao umesusiwa na waangalizi wa uchaguzi kutoka mataifa ya magharibi, ambao wanasema uchaguzi huo hautakuwa wa haki na huru.

Rais Yahya Jammeh ambaye alinyakua mamlaka kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi miaka kumi na saba iliyopita, anatarajiwa kushinda katika uchaguzi huo na kuliongoza taifa hilo kwa muhula mwingine wa miaka mitano.

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi, ECOWAS, imesema haitawatuma waangalizi wake wa uchaguzi kwa sababu ya kiwango kisichokubalika cha vitisho dhidi ya waandishi wa habari na wapinzani.

Mkuu wa tume ya uchaguzi ya Gambia amepuuza shutuma hizo akisema hazina msingi wowote.