Ripoti ya mateso yatolewa Bahrain

Mkuu wa tume huru inayochunguza mateso yaliyofanywa dhidi ya waandamanaji wanaotaka demokrasia nchini Bahrain ametoa taarifa kuhusu namna wengi miongoni mwa wafungwa walivyoteswa.

Cherif Bassiouni anasema wafungwa hao walifunikwa nyuso zao, kuchapwa viboko na kupigwa kwa miale ya umeme na walitishiwa kubakwa ili wakiri makosa.

''Mateso haya ni kinyume na sheria za Bahrain'' alieleza bwana Bassiouni, na kuongeza kuwa kumekuwa na ukosefu wa uwajibikaji katika kushughulikia suala hili.

Taarifa yake imebaini kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa Iran ilihusika na ghasia hizo, licha ya madai yaliyotolewa na vyombo vya habari vya serikali nchini Bahrain.