Mauzo ya Rolls-Royce yaongezeka

Kampuni ya kutengeneza magari ya kifahari ya Rolls-Royce imesema imeuza magari mengi mwaka jana kuliko muda wowote tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo mwaka 1906.

Kampuni hiyo, ambayo kwa sasa inamilikiwa na watengenezaji wa magari aina ya BMW wa Ujerumani, ilisema zaidi ya magari 3,500 yaliuzwa mwaka jana.

Idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 31 ukilinganisha na mauzo ya mwaka 2010.

Sehemu ya kukua kwa biashara hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa mauzo China, iliyoipiku Amerika ya Kaskazini kama soko kuu la magari hayo ya Rolls-Royce.